EWURA, TIC na TTB wapata uongozi mpya

0
206

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, ambapo amemteua Janet Mbene kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

James Mwainyekule ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Mhasibu Mkuu Tume ya Pamoja ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza kuwa Dkt. Samia pia amemteua Rashid Mchatta kuwa Skauti Mkuu Tanzania.

Mchatta anachukua nafasi ya Mwantumu Mahiza ambaye muda wa kutumikia nafasi hiyo umemalizika.

Gilead Teri ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kabla ya uteuzi huo alikuwa Mshauri Mwandamizi, Umoja wa Ulaya (EU), Copenhagen, Denmark.

Damasi Mfugale ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ambapo kabla uteuzi huo alikuwa Mshauri Mwandamizi wa Kampuni ya Afrika Chapter EBI International Consulting Group, Canada.

Pia amewateua Makamishna wa Tume wawili ambapo Caroline Mutahanamilwa ameteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Idd Mandi ameteuliwa kuwa Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza tarehe moja mwezi huu.