Wanaodhoofisha usuluhisho wa migogoro kukiona

0
206

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Eliezer Feleshi ametoa rai kwa Majaji na Mahakimu nchini kuwa tayari kuwasilisha ofisini kwake taarifa kuhusu wakili au mtendaji yeyote serikalini ambaye atathibitika kudhoofisha jitihada za serikali na mahakama za kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Dkt. Feleshi ameyasema hayo mkoani Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.

Dkt. Feleshi amesema dhamira ya serikali ni kuona migogoro inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini inatatuliwa kwa njia zitakazowawezesha wadau kumaliza tofauti zao mapema ili wakajikite katika shughuli za uzalishaji.

Amesema migogoro sio tu inatumia gharama kubwa katika utatuzi, bali inasababisha mitaji ya uwekezaji kukaa bila uzalishaji uliotarajiwa na hivyo kukwamisha maendeleo yaliyokusudiwa pamoja na kuendeleza uadui.

Aidha, Dkt. Feleshi amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwa mwaka huu iwe msingi wa kuanza mwaka wa kazi wa mahakama wa 2023 kwa kuzingatia umuhimu wa kutatua migogoro iliyopo na itayojitokeza kwa njia ya ushuluhishi.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya sheria nchini kwa mwaka huu ni umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu, wajibu wa mahakama na wadau.