Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amewaagiza wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri na majiji nchini kuhakikisha fedha za mapato zinazokusanywa kwenye maeneo yao zinatumika kuanzisha miradi ya maendeleo ya wananchi na si kwenye matumizi mengine ya ofisi.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo mkoani Kigoma wakati akizindua mradi wa kuunganisha mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato (LGICIS) na ule wa Taarifa za Kijiografia (GIS) na kuelezea kutofurahishwa na kitendo cha baadhi ya halmashauri nchini kutenga fedha ndogo ya mapato kwenye miradi ya maendeleo.
Aidha waziri Jafo ameitaka Manispaa ya Kigoma, -Ujiji kutumia mfumo wa LGICIS ili kuratibu mienendo ya kusanyaji wa mapato kwenye vyanzo vyake, lengo likiwa ni kuongeza kiwango cha mapato ya Manispaa hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa haifanyi vizuri.
Mradi wa kuunganisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato (LGICIS) na ule wa taarifa za Kijiografia (GIS) unatekelezwa katika majiji Matano na Manispaa Tatu nchini.