Wanafunzi wakamatwa kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia

0
202

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashililia wanafunzi wawili wa chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kwa tuhuma za kutishia kutekeleza unyanyasaji wa kijinsia kwa mwanafunzi wa chuo hicho kwa njia ya mitandao ya kijamii.

Waliokamtwa ni Efron Isaya (32) na Cosmas Robert (26) wote wakiwa ni wanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.

Kamanda wa Polisi, ACP Justine Masejo amesema Januari 21 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni huko chuo hicho kuliripotiwa tukio la tishio la unyanyasaji wa kijinsia kwa mwanafunzi wa chuo hicho  (jina tumelihifadhiwa) kwa njia ya mitandao ya kijamii ambapo watuhumiwa walitishia kutuma picha za utupu katika mitandao ya kijamii ikiwa mwanamke huyo asingekubali kutekeleza waliyokuwa wakitaka kutoka kwake.

Baada ya kupata taarifa jeshi hilo lilianza uchunguzi na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi hao ambapo bado Jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na mara utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.

Aidha, ametoa onyo kwa watu wachache ambao wana matumizi mabaya ya mitandao inayodhalilisha utu na heshima ya jamii ya Kitanzania ambapo amewataka kuacha mara moja tabia hiyo kwani Jeshi hilo litawachukuliwa hatua kali za kisheria.