Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe amewaomba Jaji Mkuu wa Tanzania, Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini na Kamishna Jenerali wa Magereza kufanya operesheni
safisha magereza ili kupunguza idadi kubwa ya mahabusu ambao hawapaswi kukaa
mahabusu.
Mbowe ametoa ombi hilo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na waandishi
wa habari na kufafanua kuwa gereza la Segerea lililopo mkoani Dar es salaam lina uwezo wa kukaliwa
na mahabusu 750 lakini kwa sasa kuna zadi ya mahabusu Elfu Mbili.
Kuhusu suala la Joshua Nasari kuvuliwa ubunge wa Arumeru Mashariki kutokana na
kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge, Mbowe amemtaka Nasari
kuzungumzia jambo hilo hii leo.
Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Mjini mkoani Mara, -Esther Matiko ameiomba
serikali kuwapeleka hospitali mahabusu wenye matatizo ya akili na sio kuachwa
mahabusu bila kupatiwa msaada.
Mapema mwezi huu, Mbowe na Matiko waliachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Dar es salaam baada ya kukaa gerezani kwa takribani miezi
mitatu kwa yuhuma za kuhusika na makosa mbalimbali.