Polisi yasema hali ni shwari

0
220

Jeshi la polisi nchini limeanza kufanyia kazi taarifa zilizosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii hapa nchini zinazodai kuwepo kwa uwezekamo wa kutokea kwa uhalifu wa kigaidi katika maeneo yanayopendwa kutembelewa na watu wengi nchini wakiwemo watalii.

Taarifa hizo zilianza kusambaa tarehe 25 mwezi huu, baada ya Ubalozi wa Marekani nchini kutoa tahadhari kwa raia wa nchi hiyo waliopo hapa nchini ya uwezekano wa kutokea kwa uhalifu huo.

Katika taarifa yake kwa vyombo habari Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao kama kawaida wakati jambo hilo linafanyiwa kazi.

Amewataka wananchi kutoa taarifa haraka ili ziweze kufanyiwa kazi pindi wanapoona jambo lenye kutia shaka au atakapoonekana mtu ama watu wanaowatilia mashaka kutokana na mienendo yao.

Jeshi la Polisi nchini limesisitiza kuwa hali ya ulinzi na usalama hapa nchini ni shwari na kwamba matukio makubwa yanayoweza kuleta hofu kwa wananchi yanaendelea kudhibitiwa.