Al Hilal ya Sudan kuweka kambi Tanzania

0
241

Klabu ya Al Hilal ya Sudan inakusudia kuweka kambi nchini Tanzania kujiandaa na mchezo wao wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, viongozi wa Simba ambao ndio wenyeji wa Al Hilal wamesema ni fahari kuwapokea mabingwa hao wa Sudan ambao wamekuwa na ushirikiano kwa muda sasa.

Mwenyekiti wa Simba Murtaza Mangungu amesema klabu hizo mbili zimekubaliana kushirikiana katika maeneo saba ikiwa ni pamoja na kutembeleana na kwamba tayari wameshakwenda Sudan na Al Hilal wameshafika nchini kushiriki Simba Cup.

Kikosi cha Al Hilal kitawasili nchini Januari 25 na kitacheza mchezo wake wa kwanza Januari 26, dhidi ya Namungo katika Uwanja wa Azam Complex. Mchezo wa pili utapigwa Januari 31 dhidi ya Azam FC katika Uwanja huo huo.

Aidha, Februari 5 watakipiga na Simba SC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, na baada ya hapo Februari 6 itaondoka kuelekea na Afrika Kusini tayari kuikabilia Mamelodi Februari 11.

Al Hilal ipo Kundi B ikiwa pamoja na Al Ahly, Coton Sport na Mamelod Sundowns, huku Simba ambayo nayo inashiriki mashindano hayo ikiwa kundi moja na Horoya, Raja Club Athletic na Vipers.