Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea, ameamuru kukamatwa kwa kaka yake Ruslan Obiang Nsue
kwa madai ya kuuza ndege inayomilikiwa na shirika la ndege la serikali.
Makamu wa Rais na kaka yake Ruslan ni wana wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mangue wa nchi hiyo ambaye ndiye Rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani na amehudumu kwa muda wa miaka 43.
Ruslan Obiang Nsue, mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ndege la Ceiba International, aliuza ndege aina ya ATR72-500 bila idhini ya bodi ya kampuni hiyo kwa kampuni ya Uhispania, na kuweka mfukoni fedha za mauzo hayo.
Kutokana na sakata hilo, kaka yake amependekeza kwa Rais, ambaye ni baba yao, amsimamishe kazi zake zote za serikali.
Taarifa za kuuzwa kwa ndege hiyo zimekuja kufuatia uchunguzi uliofanyika mwaka 2022 baada ya ndege kutoweka ilipokuwa ikifanyiwa matengenezo nchini Uhispania, kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya ndani.
Rais Obiang ambaye alitwaa madaraka mwaka 1979 kutoka kwa mjomba wake kufuatia mapinduzi ya kijeshi, inasemekana kuwa anamwandaa mwanae, ambaye sasa ni makamu wa Rais kurithi kiti cha Urais pindi atakapong’atuka.