Tusipende kuwapa watoto simu

0
643

Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wamiliki wa Shule na Vyuo Tanzania (TAWOSCO) Taifa, Justina Lukumay amewataka wazazi na walezi kutopendelea kuwapa watoto wao simu, kwani kwa kufanya hivyo kunawashawishi watoto kujaribu kufanya vitu visivyo wa kimaadili wanavyoviona kwenye simu na mara nyingi hufanya hivyo na watu wazima.

Lukumay ameyasema hayo katika mahojiano na TBC1 ambapo amesema vitendo vingi vya ukatili vinavyofanyika dhidi ya watoto na wanafunzi vinafanywa na watu wazima ambao ni ndugu au jamaa wa karibu na watoto hao na kwamba wamepanga kuzunguka nchi nzima kutoa elimu dhidi ya ukatili huo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TAWOSCO Taifa, Christa Rweyemamu amesema kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanafunzi vinasababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo mmomonyoko wa maadili, kukosekana kwa hofu ya Mungu, utandawazi na wazazi kutozungumza na watoto wao.

“Nafikiri ni sisi wazazi kujaribu kukaa chini na watoto na kuwaelewesha namna ya kujilinda, tusiwafiche, kwamba hawa ni wadogo, Watoto siku hizi wanapevuka haraka sana… Ukiongea nae ukamfanya rafiki yako, hata akipata shida atakueleza, kwa sababu wale wanaofanya vitendo hivi wanawatisha, nitakuua, nitakufanya hivi,” amesema Rweyemamu

Januari 20, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kongamano la TAWOSCO ambalo linalenga kujadili masuala ya ukatili dhidi ya wanafunzi na namna ya kujilinda.

Uzinduzi huo utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) mkoani Dar es Salaam.