Serikali yamaliza mgogoro wa ardhi wa miaka 15

0
247

Serikali imeumaliza mgogoro wa matumizi ya ardhi wilaya Mbarali mkoani Mbeya uliodumu kwa miaka 15 ambao ulihusisha wakazi wa wilaya hiyo katika eneo la Bonde la Usangu dhidi ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Akizungumza katika kikao na wadau waliowekeza katika Bonde la Usangu wakiwemo wakulima wa mashamba ya mpunga, mashine za kukoboa mpunga na wafugaji katika vitalu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye Tangazo la Serikali namba 28 ambayo itawawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji endelevu.

Amesema marekebisho ya tangazo hilo yatawezesha baadhi ya vitongoji vilivyokuwa vimetangazwa awali kuwa ndani ya hifadhi kuachwa nje ya mipaka ikiwemo kutoa eneo la hekta 74,000 kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

Amesema kuwa Serikali inataka kuhakikisha Wilaya ya Mbarali inaendesha shughuli za kilimo kitaalam na kwa tija. “Tumeona maendeleo makubwa na ujenzi wa viwanda vya mtu mmoja mmoja na vikundi, Serikali inataka kuona shughuli hizo zinakuwa endelevu, tunataka mpanue viwanda vyenu na mzalishe zaidi.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeamua kuitoa nje ya hifadhi Ranchi ya Usangu kwa ajili ya shughuli za ufugaji wa kisasa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula amesema kuwa maeneo ambayo yameondolewa katika hifadhi watahakikisha mpango bora wa matumizi ya ardhi unawekwa ili wananchi waweze kufanya kile ambacho kimepangwa kufanyika kwa wakati huo.