Tanzania kuendeleza uhusiano na Russia

0
474

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Russia ulioongozwa na Mjumbe maalum wa Rais wa nchi hiyo katika masuala ya Afrika ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Mikhail Bogdanov Ikulu jijini Dar es salaam.

Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemshukuru Rais Vladimir Putin wa Russia kwa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi hiyo na amemhakikishia kuwa serikali inatambua umuhimu wa uhusiano huo na kwamba itauendeleza na kuukuza zaidi hususani katika masuala ya biashara, uwekezaji, utalii na utoaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na miundombinu.

“Naomba ufikishe ujumbe wangu kwa Rais Putin kuwa Watanzania wanaipenda Russia na tunamkaribisha kuja kutembelea nchi yetu pamoja na wananchi wengine wa Russia, tunawakaribisha pia wawekezaji waje wawekeze katika fursa mbalimbali zilizopo hapa Tanzania kwa manufaa yetu sote”, Rais Magufuli amemueleza Bogdanov.

Kwa upande wake Mjumbe huyo maalum wa Rais wa Russia katika masuala ya Afrika ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mikhail Bogdanov ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kasi nzuri na maendeleo iliyoyapata katika kipindi kifupi na amebainisha kuwa Russia imedhamiria kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

Bogdanov amesema kuwa Russia ina mpango mahususi wa kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika kuongeza kasi ya maendeleo na kwamba hivi karibuni Tanzania na nchi hiyo zitatiliana saini makubaliano ya kuanzisha tume ya pamoja ya ushirikiano katika biashara, uwekezaji na uchumi ili rasilimali na fursa zilizopo katika pande zote zitumike kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa mazungumzo baina ya Rais Magufui pamoja na Waziri Bogdanov na ujumbe wake yamekwenda vizuri na kwamba Tanzania inatarajia Tume ya pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Russia itasaidia kukuza uchumi kupitia madini, gesi na utalii hasa wakati huu ambapo nchi hiyo imeitangaza Tanzania kuwa nchi yenye vivutio bora vya utalii duniani.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi Tanzania nchi Russia Meja Jenerali Mstaafu Simon Mumwi na Balozi wa  Russia nchini Tanzania, – Yuri Popov.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu wa Tanzania na Misri wanaoshughulikia ujenzi wa uwanja wa michezo katika jiji la Dodoma, uwanja unaotarajiwa kujengwa kwa msaada wa Mfalme Mohammed VI wa Morocco.

Balozi wa Morocco nchini aliyeongoza ujumbe wa wataalamu kutoka Morocco, -Abdelilah Benryane amesema kuwa pamoja na kuzungumzia uhusiano mzuri wa Tanzania na Morocoo, wamejadiliana kuhusu utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa wakati wa ziara ya Mfalme Mohammed VI wa Morocco hapa nchini mwaka 2016 ikiwemo ujenzi wa Msikiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa jijini Dar es salaam na kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa  uwanja huo utakaojengwa katika eneo la Nanenane kando ya barabara ya Dodoma – Morogoro, utajengwa kwa mfano wa mlima Kilimanjaro na utakuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji kati ya Elfu 85 na Laki Moja na Tano.