Kamati ya waamuzi ya Shirikisho la
Soka Barani Afrika (CAF) imetaja majina ya waamuzi 29 wakiwemo watatu wa kike
watakaochezesha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri
chini ya miaka 17 zitakazofanyika hapa nchini mwezi Aprili mwaka huu.
Katika orodha hiyo wamo waamuzi wa
Kike Watatu ambapo itakuwa mara ya kwanza, kwa waamuzi wa kike kuchezesha
fainali hizo na watahudhuria mafunzo maalum yatakayoanza Machi 31 hadi Aprili 4
mwaka huu nchini Morocco.
Waamuzi waliopata bahati hiyo ni
Jonesia Rukyaa kutoka Tanzania ambaye ni mwamuzi pekee wa kike katika orodha ya
waamuzi 15 wa katikati waliotangazwa.
Wengine ni waamuzi wasaidizi Mary Njoroge kutoka Kenya na Lidwine
Rakotozafinoro kutoka Madagascar ambao ni waamuzi pekee wa kike kwenye orodha
ya waamuzi wasaidizi 14 waliotangazwa.
Mataifa yatakayoshiriki fainali hizo zitakazoanza kutimua vumbi Aprili 14 hadi
28 mwaka huu jijini Dar es salaam ni wenyeji Tanzania, Nigeria, Angola na
Uganda yaliyopangwa Kundi A, wakati Guinea, Morocco, Senegal na Cameroon zikiwa kundi B.