Shule ya Samia Suluhu Hassan kuanza Julai 2023

0
149

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Januari 6, 2023 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambayo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai 2023.

Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 4 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo awamu ya kwanza ya mradi huo ilianza Aprili 6, 2022 na inatarajiwa kukamilika Januari 30, 2023, ikitumia shilingi bilioni 3 na jumla ya majengo 22 yanajengwa

Majaliwa amesema shule hiyo itakapokamilila itapokea wanafunzi 1080 ambapo awamu ya kwanza itapokea wanafunzi 600 na awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 1 itapokea wanafunzi 480.

Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa madarasa 10 yenye ofisi za walimu 3, chumba cha TEHAMA, maktaba, nyumba 4 za walimu na mabweni 4.

Waziri Mkuu amesema Rais Samia ameamua kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike ili kumpunguzia changamoto zilizowakabili na ndio maana ameamua kujenga shule za wasichana nchi nzima. “Si kwamba amemtenga mtoto wa kiume hapana, ameamua kwenda nao wote.”