Rais Samia afanya mabadiliko ya Viongozi mbalimbali

0
216

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya nafasi za uongozi katika Serikali ambapo amemteua Balozi Hussein Kattanga kuwa Balozi wa Tanzania mjini New York, nchini Marekani na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa.

Balozi Kattanga anachukua nafasi ya Balozi Profesa Kennedy Gaston ambae uteuzi wake umetenguliwa. Kabla ya uteuzi huu balozi Katanga alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Aidha, Rais amemteua Dkt. Moses Kusiluka kuwa Katibu Mkuu Kiongozi ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu Ikulu.

Pia, Rais Samia amemteua Kamishna Diwani Athuman kuwa Katibu Mkuu Ikulu. Kabla ya uteuzi huo Kamishna Diwani alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Said Masoro ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi wa Shughuli za Ndani wa Idara ya Usalama wa Taifa.