Wananchi kupewa elimu ya kutumia taarifa za Sensa

0
125

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, Anne Makinda amesema kwa sasa jitihada zinazoendelea ni kutengenesa Tanzania mpya ambayo watu wake wanazungumza, wanajitambua na wanajua kilichopo ndani ya eneo lao.

Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania juu ya maendeleo ya mchakato wa sensa amesema nguvu kubwa inatumika kuwafundisha wananchi matumizi ya taarifa za matokeo ya sensa ya watu na makazi kusudi waweze kuzitumia taarifa hizo kwa ajili ya maendeleo.

Katika moja ya hatua za kufundisha matumizi ya taarifa hizo Makinda amesema kwa sasa mafunzo yameanza kwa waratibu wa sensa ngazi ya mkoa na wilaya, na kuwa mafunzo hayo yatashushwa hadi ngazi ya kitongoji na kumfikia mwananchi wa kawaida.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwafumbua wananchi macho kufahamu sababu za wao kuhesabiwa ambapo ufahamu huo utaibua fursa za kufanyika tafiti mbalimbali pamoja na watu kuzungumza na kujadili yaliyopo kwenye maeneo yao.

Makinda amesisitiza ipo haja ya watu kuzungumza, kujadili na kuchambua taarifa za eneo lao ambapo wananchi watafundishwa namna ya kutafsiri matokeo ya sensa kwa kuwa taarifa hizo ni mali yao.