TPA kuhudumia Makontena pindi TICTS itakapoondoka

0
231

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Juma Kijavala amesema mkataba wa kampuni inayohudumia utoaji wa mizigo bandarini, TICTS, unatarajia kufikia ukingoni Desemba 30 ambapo shughuli za kampuni hiyo zitafanywa na TPA mpaka hapo serikali itakapopata mbia mpya ama kuamua vinginevyo, huku akiwahakikishia wafanyakazi wa kitengo hicho kuwa ajira zao zipo salama.

Ameyaeleza hayo Bagamoyo mkoani Pwani katika kikao na waandishi wa habari wanaotoka katika mikoa yenye bandari, kikao kilicholenga kuwawezesha waandishi wa habari kufahamu shughuli za bandari.

TICTS ambayo imehudumu katika Bandari ya Dar es Salaam kwa miaka 22 sasa, iliundwa kwa ajili ya kuendesha kitengo cha makasha na kuboresha utendaji ili kuongeza mchango wa sekta ya bandari katika uchumi wa taifa, pamoja na kupunguza gharama za kuhudumia shehena za makasha zinazopita bandarini ili kuhimili ushindani na nchi jirani.

Aidha, lengo jingine ni kuvutia shehena za ndani na nje ya nchi zinazopita katika bandari hiyo na kuingiza teknolojia mpya na kuwawezesha wazawa kupata mbinu mpya za usimamizi na uongozi wa bandari.

Wakati huo huo, Kijavala amesema TPA inalenga kuongeza idadi ya shehena ya mizigo kutoka tani milioni 17.913 mpaka kufikia tani milioni 47.095 ifikapo mwaka 2045

Amesema lengo la kufanya maboresho ni kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa shindani, huku akiongeza kuwa TPA imefanya maboresho kadhaa ikiwemo ujenzi wa magati pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuendelea kuvutia wadau wa forodha duniani kutumia bandari za Tanzania kupitisha mizigo yao.