TAKUKURU kuwachunguza waliochoma nyaraka

0
100

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Mhasibu wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga mkoani Rukwa, Eric Rutyamirwa na Mkufunzi wa chuo hicho Godfrey Msenuka ili iwachunguze kwa tuhuma za kuchoma moto taarifa za mradi wa ujenzi wa chuo hicho.

Rutyamirwa na Msenuka ambaye alikuwa katibu wa ujenzi, wanadaiwa kuchoma moto nyaraka hizo na hivyo kupoteza kumbukumbu za ujenzi wa mradi huo ambao manunuzi ya vifaa vya ujenzi yanadaiwa kufanywa mara tatu zaidi ya gharama halisi.

Waziri Mkuu Majaliwa amewakabidhi watendaji hao kwa TAKUKURU baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho cha Ualimu Sumbawanga.

“Nyaraka ziliungua ndani ya ofisi ya Mhasibu huku chanzo cha moto bado hakijajulikana, lakini mfumo wa umeme haukuwa na hitilafu ulikuwa salama hata baada ya tukio la moto kutokea.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Aidha, amehoji ni kwanini mhasibu wa chuo hicho alijipa kazi ya kutunza nyaraka za ujenzi wa chuo kinyume na taratibu kwa sababu aliyepaswa kuwa na nyaraka hizo ni Katibu wa Kamati ya ujenzi, hivyo ameagiza wote wachunguzwe.

Ujenzi wa mradi wa chuo cha Ualimu Sumbawanga
unaojengwa kwa awamu mbili unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 7.1 hadi kukamilika kwake na tayari serikali imetoa shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya awamu ya kwanza.

Ulianza mwezi Agosti mwaka 2021 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka 2023.