Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa kilimo utakaohudhuriwa na viongozi, watu mashuhuri na wadau wapya elfu tatu wa kilimo.
Uamuzi huo umetangazwa na Waziri Mkuu mstaafu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn katika Jukwaa la Mtandao wa Chakula Afrika (AGRF) nchini Marekani.
Dkt. Samia amesema anatarajia mkutano huo utaendeleza uimarishaji wa mifumo ya chakula na kilimo katika vipaumbele vya serikali, kupeana taarifa na kutumia teknolojia ya kisasa kwa ajili ya mifumo imara ya chakula.
Ameongeza kuwa wadau mbalimbali watakaohudhuria mkutano huo wataweza kujadili namna ya kuimarisha biashara miongoni mwa miji mbalimbali ili kuchangia usalama wa chakula, ukuaji na uvumilivu.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema lengo la mkutano huo mkubwa wa kilimo ni kushawishi nchi zote juu ya ajira kwa vijana ambapo kila nchi barani Afrika itaweka wazi mikakati yake ya ajira hizo na namna ya kufanikisha.
Katika kuimarisha shughuli za kilimo, serikali ya Tanzania imeongeza bajeti yake karibu mara nne katika sekta hiyo kutoka dola milioni 126.7 za kimarekani kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia dola milioni 411.2 za kimarekani kwa mwaka 2022/2023
Rais Samia Suluhu Hassan yupo nchini Marekani kuhudhuria mkutano wa siku tatu wa wakuu wa nchi za Afrika na Marekani utakaohusu masuala mbalimbali ya kimaendeleo pamoja na mikutano mengine ya kimkakati.