Mlinzi wa timu ya Ajax Amsterdam ya nchini Uholanzi na timu ya Taifa ya Argentina – Nicolas Tagliafico amesema kuwa timu yake ya taifa inashindwa kumtumia vizuri nyota wa Taifa hilo Lionel Messi ndiyo maana haifanyi vizuri na hata Messi mwenyewe hafanyi vizuri akiwa na timu hiyo ya Taifa.
Messi akiwa na timu yake ya FC Barcelona ni miongoni mwa wachezaji wachache wenye mafanikio makubwa, akishinda mataji yote kwa ngazi ya klabu huku pia akihesabika kuwa mchezaji mwenye mwendelezo wa kiwango kizuri kwa zaidi ya mwongo mmoja tangu atambulike kwenye ulimwengu wa soka.
Tofauti na anapokuwa kwenye timu ya Taifa, Messi ameshindwa kulipa mafanikio Taifa lake licha ya kuwa mfungaji bora wa timu ya taifa akiwa na mabao 65 ndani ya michezo 128 ambapo hajatwaa taji hata moja.
Sasa Nicolas Tagliafico ambaye ni mchezaji mwenzie na Messi kwenye timu ya Taifa anasema ni wazi wameshindwa kuutumia ubora wa Messi kwa sababu hawachezi kwenye mfumo unaomfanya nyota huyo awike na kuisaidia timu ya Taifa.
Beki huyo anasema kama sehemu ya suluhisho inatakiwa kutafutwa wazo ama kocha atakayemfanya Messi atambe kwenye timu ya taifa kama anavyotamba kwenye klabu yake ya FC Barcelona.