Jeshi la Polisi lapongezwa

0
729

Rais John Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi nchini kwa utendaji mzuri.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo Ikulu jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Mawaziri Mawili, Balozi mmoja na Makamishna kadhaa wa Jeshi la Polisi nchini.

Hata hivyo Rais Magufuli ameeleza masikitiko yake kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watendaji wa Jeshi la Polisi nchini wasiotekeleza majukumu yao kikamilifu ambao wamekua wakilichafua jeshi hilo.

Rais Magufuli amewaagiza Makamishna hao wapya wa Jeshi la Polisi nchini kujenga taswira nzuri ya Jeshi hilo na kwa wale wanaoenda kinyume na maadili wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Amesema wakati umefika kwa uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi nchini kutowarejesha Makao Makuu Makamanda wa polisi wa mikoa ambao hawajatekeleza vizuri majukumu yao na badala yake wawekwe chini ya Makamanda wengine wa Polisi wa mikoa.

Kuhusu mabadiliko madogo aliyoyafanya katika Baraza la Mawaziri, Rais Magufuli amesisitiza kuwa ni ya kawaida na lengo lake ni kuimarisha utendaji kazi

Mawaziri walioapishwa ni Profesa Palamagamba Kabudi anayekua Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitokea wizara ya Katiba na Sheria na Balozi Augustine Mahiga aliyekua Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na amehamia wizara ya Katiba na Sheria.

Mwingine aliyeapishwa ni Balozi Yahya Simba anayekwenda kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhiriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma na Spika wa Bunge Job Ndugai.