Rais ataka mikakati zaidi mapambano ya Ukimwi

0
81

Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza
Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) pamoja na wizara ya Afya kuzidisha mapambano zaidi dhidi ya virusi vya Ukimwi.

Rais Samia ametoa agizo hilo mkoani Lindi, wakati wa kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ukimwi Duniani .

Amesema ni lazima mikakati hiyo ilenge katika kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi, kusisitiza matumizi ya dawa kwa wanaoishi na VVU pamoja na kuondoa unyanyapaa.

Kwa upande wa serikali Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi ili kuhakikisha mikakati yote inafanikiwa.

Pia amesisitiza ushirikiano wa serikali na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya Ukimwi, kwani ushirikiako huo ndio uliofanikisha kupungua kwa maambukizi mapya ya Ukimwi hapa nchini.

Wakati wa kilele hicho cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Rais Samia amezindua rasmi Mkakati wa Taifa wa miaka mitano wa mapambano dhidi ya Ukimwi, mkakati ambao unatekelezwa katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2026.

Kauli mbiu ya kitaifa ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mwaka huu ni Imarisha Usawa.