Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri nchini kutumia fedha za makusanyo ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo, badala ya kusubiri fedha kutoka serikali kuu pekee.
Majaliwa ametoa agizo hilo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya sekondari ya Mwandege iliyopo wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mkuranga, Mwantumu Mgonja kutenga shilingi milioni 120 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la utawala katika shule hiyo ifikapo mwezi Januari mwaka 2023.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba hivyo vya Madarasa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imejipanga vizuri kuwahudumia watanzania ili kusaidia kuchochea shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
“Huu ni wakati wa kufanya kazi, nimeridhika na viwango vya ujenzi wa vyumba madarsa katika shule hii, endeleeni kusimamia viwango kwenye miradi mingine, twende na matakwa ya Rais wetu na kumsadia kutimiza maono yake ya kuwahudumia watanzania.” amesema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Majaliwa, leo ameanza ziara ya kikazi mkoani Pwani, kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na watumishi wa umma wa mkoa huo.