Waziri Mbarawa: Ndege ilizunguka dakika 20

0
168

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision iliyotokea tarehe 6 mwezi huu Bukoba mkoani Kagera imeonesha kulikuwa na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyoilazimu ndege hiyo kuzunguka angani kwa muda wa dakika 20.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo alikua akitoa ripoti hiyo ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision iliyosababisha vifo vya watu 19, huku wengine 24 wakiokolewa.

Kuhusu wavuvi kushiriki katika zoezi la uokoaji Waziri Mbarawa amesema, mwongozo na taratibu za kimataifa pamoja na mkataba wa kimataifa wa ufuatiliaji na uokoaji unaruhusu watu waliopo katika eneo la ajali kuwajibika na zoezi la uokoaji.

Amewataka watanzania kufuata taarifa rasmi zinazotolewa na serikali na kuepuka upotoshaji unaoweza kujitokeza na kuibua taharuki.

Ripoti hiyo ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision imetolewa kwa kushirikisha wataalam kutoka nchini Ufaransa na wa hapa nchini.

Ripoti kamili kuhusu ajali hiyo itatolewa baada ya kipindi cha miezi 12.