Dkt. Mpango : Toeni taarifa za wahalifu

0
108

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewataka wananchi wa mkoa wa Tanga kuwabaini na kutoa taarifa za watu wanaoingia mkoani humo kwa lengo la kufanya uhalifu.

Makamu wa Rais ameyasema hayo mara baada ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anthony wa Padua Jimbo Katoliki Tanga.

Amesema jiographia ya mkoa wa Tanga inatumika kama njia ya kupokea watu mbalimbali ambao kati yao wapo wanaofanya uhalifu.

Pia Dkt. Mpango ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Tanga kuendelea kutunza mazingira, ili kuepuka athari zinazoendelea kujitokeza hivi sasa ikiwemo ukosefu maji pamoja na upungufu wa chakula.

Amewasihi viongozi wa dini nchini kuendelea kuwasisitiza waumini wao juu ya maandiko matakatifu yanayoagiza kuilinda dunia ikiwemo kutunza mazingira.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango anaendelea na ziara yake mkoani Tanga ambapo pamoja na mambo mengine anakagua shughuli mbalimbali za maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.