Nape: TRA msitumie nguvu kukusanya kodi

0
211

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetakiwa kukusanya kodi kwa kutumia taaluma na sio kutumia nguvu.

Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walipa kodi bora mwaka 2021/2022.

“Wengi walisema tukifunga vikosi kazi ‘task force’ hatutafaulu ukusanyaji wa mapato, lakini hapa nawatangazia tumeweza kukusanya kodi bila kutumia nguvu.” amesema Waziri Nape

Amesema serikali ya awamu ya sita imekuwa sikivu na itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wanaolipa kodi kwa hiari bila shuruti na itahakikisha inapunguza changamoto wanazokabiliana nazo.

“Tabia ya vitisho kwa wafanyabishara si sawa, na hii tabia inafanywa na watu wa TRA wadogo wadogo, sasa hawa wadogo wadogo wasipake matope kazi nzuri inayofanywa na TRA na tuzo hizi zitaongeza hamasa kwa wengine kulipa kodi kwa uaminifu na kwa wakati.” amesema Waziri Nape

Ameiagiza TRA kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya fursa za uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Alphayo Kidata amesema, utoaji wa tuzo hizo umezingatia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja utunzaji wa kumbukumbu za mlipa kodi, ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati pamoja na ushirikiano mzuri wakati wa ukusanyaji wa kodi.