Watendaji TCCIA wanolewa India

0
151

Tanzania imeshauriwa kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia rahisi za uzalishaji pamoja na rasilimali watu, ili kusaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Taasisi ya Uongozi ya Jaipuria nchini India Dn Pandey, alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki mbili yanayolenga kuongeza ujuzi katika nyanja ya teknolojia, utalii na uzalishaji.

Mafunzo hayo yanafadhiliwa na serikali ya india na yanatolewa kwa wafanyakazi wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA ).

Pandey amesema India imefanikiwa kuwa na uchumi mkubwa unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola trilioni tatu za kimarekani kwa kuwa iliwekeza zaidi kwenye ujuzi, elimu na teknolojia rahisi za uzalishaji.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania anayeshughulikia biashara DKt. Meshack Kulwa amesema, mafunzo hayo yatawawezesha kufikia azma ya serikali ya kuifanya sekta binafsi kuwa injini ya uchumi .

Ujumbe wa watu 29 kutoka Tanzania chini ya mwamvuli wa TCCIA, upo nchini India kwa ajili ya mafunzo ya wiki mbili yanayolenga kuwaongezea uwezo wa namna bora ya kusimamia na kuendesha biashara kisasa kupitia teknolojia, lengo likiwa ni kuiwezesha Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini kuwa na uwezo wa kufanya biashara za kimataifa.