Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza jamaa zao katika ajali ya barabarani, iliyotokea wilayani Mbozi mkoani Songwe na kusababisha vifo vya watu 19.
Ajali hiyo imetokea usiku wa Alhamisi Februari 21 mwaka 2019 katika mteremko wa mlima Senjele ambapo lori lililokuwa likisafiri kutoka Tunduma kwenda Mbeya Mjini lililigonga basi la abiria kwa nyuma, kisha basi hilo likaminywa katikati baada ya kuligonga lori jingine lililokuwa mbele yake na kusababisha vifo vya watu wote 18 waliokuwemo ndani ya basi pamoja na dereva wa lori lililogonga basi hilo.
Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemas Mwangela, kufikisha salamu zake za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya watu hao na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu wote mahali pema peponi, Amina.
Aidha, Rais Magufuli amezitaka mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani mkoani Songwe kufanya uchunguzi wa ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili pamoja na kujipanga vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa mkono wa pole kwa familia ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt Hamisi Kigwangalla ambaye amefiwa na motto wake Zul Hamis Kigwangalla Alhamisi Februari 21 mwaka huu jijini Dar es salaam.
Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wamefika nyumbani kwa familia ya Dkt Kigwangalla Mikocheni jijini Dar es salaam na kukutana na baadhi ya wanafamilia wakiwa katika maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Nzega mkoani Tabora ambapo mazishi yatafanyika baadaye hii leo.