Rais Samia Suluhu Hassan ameziagiza mamlaka husika kukomesha upotevu wa maji unaosababishwa na ufugaji holela na shughuli za kijamii zinazoendelea kando ya vyanzo vya maji.
Rais Samia ametoa agizo hilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Amesema tatizo la maji kwa mkoa wa Dar es Salaama limetokea mwaka 2021 na mwaka huu huku utafiti ukibaini matumizi mabaya ya mto Ruvu ndio chanzo.
Rais amesema tafiti zimeonesha wafugaji wamekuwa wakinywesha ng’ombe zaidi ya elfu tano katika mto huo ambapo ng’ombe mmoja anatumia takribani lita 45 za maji kwa siku.
Amesema hali hiyo husababisha maji mengi kuisha kabla hayajafika katika mitambo kwa ajili ya kusafishwa ili kutumika majumbani.
Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, maji ya mto Ruvu pia huchepushwa na mabwawa yamejengwa kando ya mto huo na kusababisha kupungua kwa kina cha maji katika mto huo.