Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson ameitaka Serikali kuangalia upya utaratibu uliowekwa katika baadhi ya maeneo nchini wa kuyazuia magari ya abiria kufanya shughuli za usafirishaji nyakati za usiku kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo ya kiuchumi.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Novemba 10, 2022 wakati aliposhiriki semina kwa Wabunge kuhusu usalama barabarani, iliyoandaliwa na wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kufanyika katika ukumbi wa Msekwa Bungeni jijini Dodoma.
Amesema ni lazima ifike wakati Wananchi waweze kufanya shughuli zao muda wote na kuondoa dhana iliyozoeleka ya magari ya abiria kuwekewa vikwazo vya kufanya kazi kwa sababu zizisokuwa rasmi wakati magari mengine yakiwemo ya mizigo yanaruhusiwa.
“Kuna shida gani ya kuzuia gari ya abiria kusafiri usiku?.Tunatamani nchi yetu kuchangamka zaidi kiuchumi, sasa kwanini magari haya yawe na zuio wakati magari mengine yanaruhusiwa kusafiri hadi usiku. Kama ni changamoto ya miundombinu basi ishughulikiwe na shughuli zifanyike.” amesisitiza Dkt. Tulia.