Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limesema litapunguza miruko ya ndege zake pamoja na kufuta baadhi ya safari ili kutoa muda wa matengenezo ya injini.
Taarifa ya ATCL imesema kuwa, uamuzi huo unatokana na changamoto za kiufundi kote duniani kwenye injini aina ya PW1524G-3 zinazotumika katika ndege aina ya Airbus A220-300.
Kwa mujibu wa Shirika la Ndege la Tanzania, uamuzi huo wa kupunguza miruko ya ndege pamoja na kufuta baadhi ya safari za ndege za ATCL ni wa muda mfupi ili kutoa muda kwa watengenezaji wa injini hizo kushughulikia matatizo yaliyopo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa kuzingatia matakwa ya usalama, ATCL imekuwa ikifuata maelekezo ya kitaalamu ili kutoa huduma bora na ya usalama, ndio maana wakati mwingine inazitoa ndege katika mzunguko kukidhi matakwa ya watengenezaji wa injini hizo.