Shabiby aishauri Serikali ijenge barabara za kulipia

0
162
Mbunge wa jimbo la Gairo mkoani Morogoro, Ahmed Shabiby akizungumza katika kikao cha saba cha mkutano wa tisa wa bunge la 12.

Mbunge wa jimbo la Gairo mkoani Morogoro, Ahmed Shabiby ameitaka Serikali kujenga barabara kwa kushirikiana na sekta binafsi, na kama haiwezi kufanya hivyo ijenge barabara kwa mkopo, kisha barabara hizo ziwe za kulipia ili ipate fedha za kurejesha mkopo.

Akichangia mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024 Shabiby amesema, Serikali haiwezi kujenga barabara zote kwa fedha zake za ndani.

“Hatuwezi kujenga wenyewe, dunia nzima inajenga kwa PPP [Ushirikiano na Sekta Binafsi], na kama PPP hatupati basi kopeni, kukopa sio dhambi […] Kopeni halafu wekeni road toll [tozo za barabara].” amesema Shabiby

Akitoleo ufafanuzi kuhusu ujenzi wa barabara, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba amesema kuwa, Serikali tayari inalifanyia kazi suala la ujenzi wa barabara kwa kushirikiana na sekta binafsi.

“Serikali imetoa tangazo la kufanya kazi na wapo walioandika barua kuonesha nia kwa utaratibu huo anaousema wa PPP tutajenga barabara ya Kibaha mpaka Morogoro, njia za kutosha kama za majuu kule,” ameeleza Dkt. Nchemba

Aidha, amesema utaratibu huo hautaishia kwenye barabara hiyo, bali utahusisha nyingine ikiwemo barabara inayoanzia Mbulu mpaka Maswa kupitia Sibiti, barabara inayotoka Handeni hadi Singida na Arusha hadi Kongwa.