TET, OUT wapeleka Kiswahili Malawi

0
159

Serikali imeitaka taasisi ya Elimu Tanzania (TET) pamoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kutumia fursa ya kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Malawi ili kuikuza lugha hiyo katika nchi za Afrika na dunia kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa mjini Lilongwe nchini Malawi na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo wakati wa kikao cha Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole pamoja na wakuu taasisi hizo mbili.

Profesa Nombo amesema TET na OUT wana uwezo wa kuifanya lugha ya Kiswahili kufahamika na kwa kutumia wataalamu walionao suala hilo litawezekana kufanyika kwa haraka.

Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole amesema, tayari wamefanikiwa kuanzisha ushirikiano huo mzuri ambao utasaidia kukuza lugha ya kiswahili nchini humo.

Balozi Polepole ameishukuru TET, OUT na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kukubali kufanya ushirikiano huo wenye lengo la kuikuza lugha ya Kiswahili.

Ujumbe wa TET na OUT upo nchini Malawi kwa ziara ya kikazi kwa mwaliko wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo.