Nahodha wa Klabu ya soka ya Yanga Bakari Mwamnyeto amesema yeye na wachezaji wanzake wapo kamili kuwakabili wapinzani wao Club Africain ya Tunisia.
Mchezo huo wa marudiano baina ya miamba hiyo miwili utapigwa leo saa mbili usiku katika dimba la Stade Olympic Rhades mjini Tunis.
Mchezo wa mkondo wa kwanza baina ya timu hizo ulipigwa Novemba 2 mwaka huu katika dimba la Benjamin Mkapa na ulimalizika kwa sare ya kutofungana.
Nahodha Mwamnyeto amesema wapo tayari kucheza kwa asilimia 100 ili kuhakikisha wanapata matokeo ya kuwapeleka hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Katika mchezo huo wa leo, Yanga watamkosa mlinzi wake wa kulia Djuma Shaban ambaye hakusafiri na timu kutokana na majeraha.
Yanga inahitaji sare ya magoli ama ushindi wowote ili kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.