Majaliwa Jackson, kijana ambaye alisaidia kuokoa watu 24 kutoka ndani ya ndege iliyopata ajali mkoani Kagera, anatarajiwa kuanza mafunzo ya zimamoto na uokoaji na yale ya uaskari katika chuo cha Zimamoto na Uokoaji kilichopo Chogo wilayani Handeni mkoani Tanga.
Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaii Kamishna Jenerali John Masunga amesema tayari Majaliwa amepokelewa na jeshi hilo, hivyo agizo la Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Rais Samia Suluhu Hassan limetekelezwa.
Hapo jana wakati wa shughuli ya kuaga miili ya watu 19 waliofariki dunia katika ajali hiyo ya ndege, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Rais Samia ameagiza kijana huyo aingizwe kwenye Jeshi hilo la Zimamoto na Uokoaji ili apatiwe mafunzo zaidi.