Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imesema kuwa haijapata ushahidi wowote unaoonesha kwamba Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ilileta kiburi na kukwamisha utendaji wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda.
Kamati imetoa taarifa hiyo bungeni jijini Dodoma baada ya kufanya mahojiano na HESLB pamoja na Waziri wa Elimu ikiwa ni maelekezo ya Spika wa Bunge aliyoyatoa juma lililopita baada ya Profesa Mkenda kusema kuwa bodi hiyo imeweka ukinzani kwa kamati iliyoundwa.
Kamati iliyoundwa na waziri ililenga kuchunguza utaratibu wa utoaji mikopo kwa miaka mitano iliyopita ili kubaini kuwa endapo vigezo vya utoaji vilifuatwa au kulikuwa na upendeleo kwa wanafunzi ambao hawakuwa na vigezo.
“… Mimi nilichogundua, baada ya kuunda hii tume, kamati sio tume, resistance ambayo ilikuwepo ya kuzuia isifanye kazi imenishawishi kwamba huenda kuna madudu makubwa sana katika bodi…” alisema Profesa Mkenda
Hivyo, kamati ya bunge baada ya mahojiano yake imesema kuwa baada ya hadidu za rejea kuwasilishwa bodi ya mikopo kamati ya waziri imeanza na kuendelea kufanya kazi, jambo linaloashiria kutekelezwa kwa maelekezo ya waziri.
Aidha, kamati imesema matokeo hayo yanadhihirisha kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano na mahusiano katika maeneo mawili ambayo ni ndani ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na baina ya Wizara na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini.
Hata hivyo, akizungumza bungeni baada taarifa ya kamati ya bunge, Waziri Mkenda amesema kamati hiyo inapata ushirikiano kutoka kwa bodi, na anaridhika na kasi ya uchunguzi inavyokwenda.