Mradi wa umwagiliaji bonde la Mara wajadiliwa

0
564

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameongoza majadiliano ya Tanzania na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika mradi wa umwagiliaji wa bonde la Mara.

Majadiliano hayo yamefanyika katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika mwaka 2022 jijini Abidjan, Ivory Coast.

Akizungumza katika majadiliano hayo Dkt. Mpango amesema Tanzania ni sehemu sahihi zaidi ya uwekezaji kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa ni lango muhimu zaidi kibiashara kwa nchi za Afrika Mashariki zenye watu zaidi ya milioni 300 pamoja nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) zenye watu zaidi ya milioni 450.

Amesema Tanzania ina hekta milioni 44 zilizoainishwa kwa ajili ya kilimo, na ni takribani hekta milioni 10.8 pekee zinazolimwa.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, eneo linalofaa kwa umwagiliaji linakadiriwa kuwa hekta milioni 29.4, na takriban asilimia 2.4 pekee zimetumika.

Pamoja na hayo, Makamu wa Rais ametaja juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali zenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji kama vile uboreshaji wa miundombinu ikiwemo reli, barabara, bandari, usafiri wa anga na maboresho katika upatikanaji wa nishati ya uhakika.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo wa umwagiliaji wa bonde la Mara
kwa wawekezaji, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa amesema, mradi huo unatarajiwa kuimarisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, ufugaji na uvuvi pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo katika eneo hilo.

Aidha Mndolwa amesema mradi huo utaongeza kipato kwa wakulima wadogo wanaoishi maeneo hayo pamoja na kuongeza ajira na uzalishaji wenye tija.

Mradi wa Umwagiliaji wa bonde la Mara unatarajiwa kutekelezwa katika wilaya za Serengeti, Tarime na Butiama mkoani Mara.