Bodi ya Mikopo yahojiwa na kamati ya bunge

0
305
Viongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wakiwasili katika viwanja vya bunge kwa ajili ya kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo imefika mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kufuatia agizo lililotolewa na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Novemba 1 mwaka huu.

Spika Tulia aliagiza bodi hiyo kufika mbele ya kamati hiyo kujieleza baada ya Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda kulieleza bunge kwamba bodi imekuwa ikisuasua kutoa ushiriikiano kwa kamati aliyoiunda kuchunguza utoaji wa mikopo kwa wanafunzi kwa miaka mitano iliyopita.

Akizungumza bungeni Waziri Mkenda alisema kuwa ukinzani ambao kamati imekuwa ikikumbana nao ni ishara kuwa kuna madudu mengi ndani ya bodi.

“Sasa hili la kuonesha pengine kiburi fulani ndio linalonipa shida,” alisema Spika na hivyo kuagiza “Siku ya Ijumaa, saa 7:00 wajikute ndani ya hiyo kamati.”

Spika alisema baada ya kuhojiwa na kamati, taarifa ya kamati itawasilishwa bungeni.

Akizungumza baada ya kuhojiwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa HESLB, Omega Ngole amesema wameitikia wito wa kamati lakini ni mapema sana kusema kilichoongelewa kwa sababu bado vikao vinaendelea.