Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Angellah Kairuki ameweka wazi vipaumbele vya wizara hiyo katika kipindi ambacho atakuwa anaiongoza.
Akisimama bungeni jijini Dodoma kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa na kuapishwa kushika wadhifa huo, Kairuki amesema vipaumbele hivyo vitagusa rasilimali watu, mifumo na miundombinu kwenye halmashauri.
Vipaumbele hivyo ni;
- Kujenga mifumo endelevu ya kitaasisi ambayo itaendelea kuwepo hata mawaziri wakibadilishwa.
- Kudhibiti matumizi ya miradi ya maendeleo na matumizi mengineyo katika halmashauri ili kuhakikisha taratibu za kifedha zinazingatiwa.
- Kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma kwa kujiridhisha kuwa matumizi yanayofanyika ni yale yanayohitajika.
- Ukusanyaji na ukadiriajiwa mapato. Amesema baadhi ya halmashauri hukadiria kwa viwango vya chini ili kwenye makusanyo waonekane wamevuka lengo, hivyo watapitia kila halmashauri kujiridhisha.
- Kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kukuza mapato ya halmshauri.
- Usimamizi wa utoaji wa huduma za afya, elimu na miundombinu ili kuboresha maisha ya Watanzania.
- Kujenga uwezo wa watumishi ili watekeleze vyema majukumu yao kwenye halmashauri.
Amesema ataendeleza mazuri ya watangulizi wake na kwamba watakuwa wasikivu katika kuwasikiliza wabunge.