TBC yaigusa ofisi ya DPP

0
153

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limetoa msaada wa magodoro, shuka, sabuni na taulo za kike kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ili upelekwe kwa watoto wenye uhitaji katika vituo vya kurekebisha tabia.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC Moses Chitama amesema, shirika hilo limeona ipo haja ya kutoa msaada huo kwenye vituo vya watoto vya kurekebisha tabia ili kusaidia penye upungufu.

Amesema jukumu la kusaidia watoto ni la kila mmoja, hivyo ameziomba taasisi nyingine kujitokeza na kutoa msaada kwenye vituo vya watoto vya kurekebisha tabia vyenye uhitaji.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya vituo vya watoto vya kurekebisha tabia, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Sylvester Mwakitalu amesema, msaada uliotolewa na TBC utasaidia kuwahudumia watoto waliopo kwenye vituo hivyo vya kurekebisha tabia.

Amesema msaada huo pamoja na kuupeleka kwenye vituo vya watoto vya kurekebisha tabia, pia atauelekeza zaidi kwa kundi la watoto ambao wapo magerezani na wazazi wao ambapo magereza hayo hayapo rasmi kwa ajili ya watoto.