Majaliwa atoa agizo wizara ya Maji, DAWASA

0
278

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya Maji kwa kushirikiana na sekta binafsi ihakikishe inakamilisha taratibu za utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Rufiji utakaosambaza maji katika maeneo ya mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

 Pia ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima zaidi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo mkoani Dar es Salaam, baada ya kukutana na Waziri wa Maji, viongozi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani pamoja na DAWASA kwa lengo la kujadili hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema serikali itahakikisha maeneo yote yanapata huduma ya maji na kazi ya uchimbaji visima pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya maji inaendelea ili kufikia matamanio ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikisha huduma ya maji karibu na makazi ya wananchi.

Akizungumza baada ya kukagua na kuwasha pampu ya maji katika mradi wa visima vya maji Kigamboni, Waziri Mkuu amesema visima hivyo ambavyo vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 70 kwa siku vitasaidia katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam.

Hapo jana wakati wa mjadala wa kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia, Rais Samia Suluhu Suluhu Hassan alimuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhakikisha anasimamia uunganishwaji wa maji kutoka Kigamboni kwenda maeneo mengine ya mkoa wa Dar es Salaam pamoja na kuangalia maunganisho ya maji ili kukabiliana na uhaba wa maji katika mkoa huo .