Habari ya kiingereza TBC ‘TBC NEWS’

0
203

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limeanza rasmi kutangaza taarifa ya habari kwa lugha ya kiingereza (TBC NEWS) kuanzia tarehe moja mwezi huu ambayo inatangazwa kuanzia saa 4:00 hadi saa 4:30 usiku.

Uzinduzi wa taarifa hiyo ya habari ya TBC kwa lugha ya kiingereza umefanywa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akiwa mbashara katika studio za TBC jijini.Dodoma.

Waziri Nape amesema taarifa hiyo ya habari kwa lugha ya kiingereza itaiwezesha TBC kufikisha taarifa mbalimbali za Tanzania Kimataifa.

“Habari ya TBC NEWS itaimarisha uhusiano na washirika wa maendeleo, Rais Samia Suluhu Hassan ameboresha sana uhusiano wa kimataifa na Tanzania tunapata wawekezaji. Wakati wanajifunza Kiswahili ni vema wakawa huru na kupata nafasi ya kusikiliza taarifa ya habari kwa lugha ya kiingereza ili wawe na uwezo pia wa kuelewa na kufanya maamuzi.” amesema Waziri Nape

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema ni muhimu kwa TBC kama taasisi ya umma kuiwakilisha Tanzania Kimataifa katika masuala mbalimbali kupitia taarifa ya habari kwa lugha ya kiingereza.

“Ni muhimu kwa TBC kuwafikishia hadhira ya kimataifa maudhui ya Afrika na Tanzania katika mitazamo yetu sisi.”Dkt. Ayub Rioba Chacha

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kupitia ukurasa wake wa Instagram ameipongeza TBC kwa hatua hiyo na kusema
“Ni fursa akrama kwa wanaofuatilia habari za Tanzania ilihali wakiwa hawaelewi lugha ya Kiswahili”.