Serikali imesema kuwa walicholipwa waathirika wa mabomu ya Mbagala mkoani Dar es Salaam ni kifuta machozi na sio fidia, kwani Serikali huwa haitoi fidia kwenye majanga yanayotokea.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo aliyetaka kujua nini kauli ya Serikali juu ya mapunjo ya fidia kwa wananchi walioathirika na mlipuko wa mabomu Mbagala.
“Yanapotokea majanga Mhe. Spika, huwezi ukayawekea utaratibu wa kulipa fidia, kwa hiyo hakuna utaratibu wa fidia kwa majanga, bali ambacho hutokea Serikali huweza kutoa kifuta machozi au mkono wa pole kwa familia zilizoathirika,” amesema Waziri Simbachawene akiongeza kuwa majanga yanaweza kuwa mlipuko wa magonjwa, tetemeko au matokeo ya nguvu za asili.
Amesema Serikali ilitoa kifuta machozi chenye thamani ya shilingi bilioni 17.4 kwa waathirika 12,647, ambazo zilitolewa kwa awamu sita kuanzia mwaka 2009 hadi Machi 2020, baada ya wahusika wote kujitokeza na kupewa fedha hizo.
Serikali pia iligharamia mazishi ya watu 29 waliofariki dunia kutokana na mlipuko huo uliotokea Aprili 29, 2009 katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).