Bunge: Wanafunzi wenye sifa waliokosa mikopo wapokelewe vyuoni

0
378
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda akichangia hoja wakati wa mjadala kuhusu utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Bunge limepitisha azimio la kuitaka Serikali kuweka utaratibu utakaoruhusu wanafunzi waliostahili kupata mikopo, lakini hawajapata, wapokelewe vyuoni na waendelee na masomo wakati Serikali ikifanyia kazi suala lao.

Azimio hilo limepitishwa kufuatia hoja iliyotolewa na Mbunge wa Biharamulo, Mhandisi Ezra Chilewesa kuhusu hatma ya wanafunzi wanaostahili kupewa mikopo kukosa fursa hiyo, huku wasiostahili wakipewa.

Kufuatia hoja hiyo, bunge liliahirisha shughuli zake na kujadili suala hilo na kufikia muafaka juu ya azimio hilo.

Aidha, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kufika mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii siku ya Ijumaa ili kueleza sababu za kutoipa ushirikiano kamati ya Serikali iliyoundwa kuchunguza utaratibu wa kutoa mikopo kwa miaka mitano iliyopita.

Awali, akichangia hoja ya Mbunge Chilewesa, Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda alisema kamati aliyoiunda kukosa ushirikiano wa bodi ni ishara kwamba kuna madudu ndani ya bodi na kuna haja ya kuipitia upya taasisi hiyo.