Bunge laahirisha shughuli kujadili mikopo elimu ya juu

0
340
Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhandisi Ezra Chiwelesa akitoa hoja kuhusu utaratibu wa utoaji wa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania.

Bunge limeahirisha shughuli zake ili kujadili hoja iliyotolewa na Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhandisi Ezra Chiwelesa kuhusu utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Katika hoja aliyoiwasilisha bungeni jijini Dodoma, Chiwelesa amesema kuwa wapo wanafunzi waliokidhi vigezo vya kupata mikopo, lakini hawajapewa, na hivyo kuweka mashakani hatma yao ya kuendelea na elimu ya juu.

Amesema yupo mwanafunzi wa kike aliyesoma shule ya sepondari ya Msalato kidato cha kwanza hadi cha sita akipata daraja la kwanza (Division 1) katika ngazi zote, amepangiwa kusoma udaktari ambao ada yake ni shilingi milioni 5, lakini amekosa mkopo.

Amedai kuwa hakuna ushirikiano kati ya bodi ya mikopo na Serikali, kwani hivi karibuni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda aliunda kamati ya kuchunguza utaratibu uliotumika kutoa mikopo kwa miaka mitano iliyopita, lakini akasema kamati hiyo imeshindwa kufanya kazi kwa kukosa ushirikiano kutoka bodi.