Korea kuchangia ujenzi wa chuo cha TEHAMA

0
689

Korea Kusini imekubali kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika ujenzi wa chuo cha Teknolojia ya Habari na Mawasilino (TEHAMA) nchini Tanzania.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baada ya mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Han Duck-Soo mjini Seoul.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema lengo la chuo hicho ni kuwasaidia vijana kuendeleza ubunifu wao na kuonesha namna wanavyoweza kuunda vifaa mbalimbali.

“Mpango wa Rais wetu wa kuwapa vijana shughuli za kufanya katika eneo la Sayansi na Teknolojia ni mpango ambao unaungwa mkono na Serikali ya Korea.” amesema Majaliwa

Oktoba 14 mwaka 2021 wakati Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza katika kilele cha mbio za Mwenge kitaifa kwenye viwanja vya Magufuli wilayani Chato mkoani Geita, alisema serikali inatarajia kujenga chuo bora zaidi cha kisasa cha TEHAMA ili kuongeza kasi, ubunifu na ufanisi katika matumizi ya teknolojia hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amekutana na viongozi wa kampuni ya Mirae Chemical ambao wanajenga kiwanda cha kuchakata maganda ya korosho baada ya kubanguliwa ambacho kwa mara ya kwanza teknolojia hiyo inaingia nchini Tanzania.