Mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Lupakisyo Kapange amewaomba maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwafikia wafanyabiashara waliopo nje ya miji na kuwapa elimu ya kodi, ili waweze kulipa kodi na kuongeza mapato ya serikali.
Kapange ametoa ombi hilo kwa maafisa hao wa TRA waliofika ofisini kwake kujitambulisha, kabla ya kuanza kampeni ya mlango kwa mlango yenye lengo la kuwaelimisha wafanyabiashara wa Bariadi pamoja na kusikiliza changamoto zao.
Aidha mkuu huyo wa wilaya ya Bariadi amewataka wafanyabiashara wilayani humo kutoa ushirikiano kwa maafisa hao wa TRA, ili washughulikie changamoto zinazowakabili na hivyo kuwawezesha kulipa kodi kwa urahisi.