Wamisri kuwekeza katika huduma za afya nchini

0
450

Taasisi inayojihusisha na utoaji wa huduma za afya nchini Misri ya Alameda Healthcare Group, imesaini makubaliano ya awali ya ushirikiano na wizara ya Afya katika masuala mbalimbali.

Makubaliano hayo ni kwa ajili ya kuanzisha kituo cha ushauri wa afya, kuwapa mafunzo wataalamu wa afya katika maeneo ya kibingwa, kuendesha kambi za upasuaji katika hospitali za umma na kutoa tiba kwa wagonjwa kama upandikizaji figo nchini Misri.

Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa wizara ya Afya Abel Makubi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Alameda Healthcare Group, Neeraj Mishra.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Mishra amesema ni faraja kushirikiana na wizara ya Afya katika kuboresha huduma za afya nchini Tanzania.

“Katika makubaliano haya tutaendesha kambi za upasuaji wa moyo, kupandikiza figo, upasuaji wa mishipa ya fahamu na magonjwa ya mifupa.” amesema Mishra

Tayari taasisi hiyo ya Alameda ina makubaliano na taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na hospitali ya Taifa Muhimbili na mwezi Septemba mwaka huu wataalamu wa taasisi hiyo walikuja nchini kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa.