MOI yapokea madaktari kutoka Ireland

0
275

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imepokea jopo la madaktari bingwa wa mifupa wa watoto kutoka Taasisi ya Children Health Ireland Africa (CHIA), ambao wataendesha kambi ya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa MOI kwa muda wa siku nne.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema, ujio wa madaktari bingwa kutoka Ireland ni sehemu ya mkakati wa MOI wa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kimataifa ili kuboresha huduma kwa wananachi.

“Leo tumepokea wageni kutoka nchini Ireland ambapo watakua nasi hapa kwa siku nne, watatoa huduma kwa wagonjwa ikiwemo upasuaji kwa watoto 10 wenye viungo vilivyopinda.” amesema Dkt. Boniface

Kwa upande wake afisa Uendeshaji mkuu wa Shirika la CHIA Joe Gannon amesema, ni heshima kubwa kupata fursa ya kushirikiana na hospitali ya MOI ili kuangalia namna bora ya kuboresha huduma kwa watoto.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa tiba wa Taasisi hiyo ya CHIA Dkt. Paula Llelly amesema, ushirikiano kati ya taasisi yake na MOI utakua na manufaa makubwa kwa pande zote mbili ambapo wanufaika wakubwa watakuwa wagonjwa.