Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Camillus Wambura amesema, timu maalum imeundwa kuchunguza tukio la mauaji ya watu wawili pamoja na majeruhi wawili lililotokea wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Amesema timu hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, imeundwa ili kubaini chanzo cha matumizi ya risasi za moto kati ya Jeshi la Polisi na wananchi wa kijiji cha Ikwambi lilipotokea tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, IGP Wambura amewataka askari wote walioshiriki kwenye tukio hilo kupisha uchunguzi, ili timu hiyo iweze kufanyakazi kwa uhuru.
Pia amewataka wananchi wa kijiji hicho cha Ikwambi kutoa ushirikiano kwa timu hiyo.
IGP Wambura amesema chanzo cha tukio hilo ni mgogoro baina ya wafugaji na wakulima wa kijiji hicho ambao waliwafungia viongozi wa kijiji ndani ya ofisi, jambo lililowafanya polisi kujaribu kuwaokoa viongozi hao.