Rais Samia ataka maboresho nje ya bandari ya Kibirizi

0
265

Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kujenga barabara ya lami, ili kuboresha miundombinu inayoingia katika bandari ya Kibirizi mkoani Kigoma.

Rais Samia amesema hayo wakati akisalimiana na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa makao makuu ya bandari za ziwa Tanganyika katika bandari ya Kibirizi mkoani Kigoma.

Amesema hajapendezwa na barabara pamoja na mwonekano wa eneo la nje la bandari hiyo kutokana na kuwa na vibanda vya wafanyabiashara vilivyojengwa bila utaratibu mzuri.

Kutokana na hali hiyo Rais Samia amewataka wafanyabiashara wadogo kupitia umoja wao kukubaliana na uongozi wa mkoa na wilaya, ili lijengwe soko la kisasa litakaloboresha taswira ya eneo la nje ya bandari ya Kibirizi.

Mradi wa ujenzi wa makao makuu ya bandari za ziwa Tanganyika utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 32 hadi kukamilika kwake na mpaka umefikia asilimia 66.

Utekelezaji wa mradi huo unafanyika katika bandari tatu ambazo ni bandari kuu ya Kigoma, bandari ya Kibirizi na bandari ya Ujiji.

Majengo yanayojengwa ni ofisi za utawala, upanuzi wa magati, maghala ya mizigo, jengo la abiria na ofisi nyingine za huduma muhimu kama uhamiaji, polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).